Taarifa iliyotolewa jana na EuroMed Rights imelaani matamshi rasmi na yasiyo rasmi ya viongozi wa Ufaransa yanayohujumu Uislamu na kueneza chuki dhidi ya Waislamu na kusema: Matamshi hayo yanawafanya Waislamu walio wachache nchini Ufaransa kuwa walengwa rahisi wa hujuma na mashambulizi ya makundi yenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia na magenge ya wabaguzi wa rangi, na vilevile yanahamasisha ubaguzi dhidi ya Waislamu.
Kituo hicho cha kutetea haki za binadamu kimeitaka serikali ya Ufaransa iheshimu sheria za kimataifa na za Ulaya zinazosisitiza ulazima wa kuheshimu dini zote.
EuroMed Rights pia imeitaka serikali ya Ufaransa kukomesha matamshi na misimamo ya kihasama dhidi ya dini ya Uislamu inayochukuliwa kwa malengo ya kampeni za uchaguzi.
Chuki na hujuma dhidi ya Uislamu vimeongezeka sana nchini Ufaransa hasa baada ya Rais Emmanuel Macron kutetea vitendo vya chuki hususan vile vinavyomvunjia heshima Mtume Muhammad (saw) kwa kisingizo cha uhuru wa maoni.
Waislamu katika pembe mbalimbali za dunia wamekasirishwa sana na misimamo hiyo ya Rais wa Ufaransa na kutoa wito wa kususiwa bidhaa za nchi hiyo.
Rais wa Jamhuri ya Chechnya, Ramzan Akhmadovich Kadyrov amesema Rais Macron wa Ufaransa anahamasisha ugaidi kwa kuhalalisha na kutetea vibonzo vinavyomtusi na kumdhalilisha Mtume wa Mwenyezi Mungu.
Rais wa Chechnya amesema Emmanuel Macron ni kinara wa ugaidi na mhamasisha wa uovu huo nchini ufaransa.
342/